Sunday, September 1, 2013

WAISLAMU NCHINI WAMETAKIWA KUVITUMIA IPASAVYO VYAMA VYA AKIBA NA MIKOPO-SONGEA




 PICHA NA MPENDA MVULA.

WAISLAMU nchini wametakiwa kuvitumia ipasavyo vyama vya akiba na mikopo vinavyoanzishwa katika maeneo yao kwa kujiendeleza kielimu na kiuchumi kwa sababu waislamu walio wengi bado wako nyuma kielimu na kiuchumi pia hivyo wanapaswa kuzitumia ipasavyo fursa zilizopo.

 Wito huo umetolewa na katibu mkuu wa baraza kuu la jumuiya na taasisi za kiislamu nchini Shekh Ramadhan Sanze ambaye pia ni meneja wa vyama vya akiba na mikopo vya KUTYABA  Tanzania wakati wa ufunguzi wa chama cha akiba na mikopo cha waumini wa kiislamu wa wilayani Songea mkoani Ruvuma.
Amesema waislamu walio wengi bado wako nyuma kielimu na kiuchumi pia kwa sababu ya hali ya halisi ya kihistoria na kuamini kuwa ujasiriamali wenye historia kukopeshwa na kulipa kwa riba na imani ya uislamu ni vitu viwili tofauti hivyo baraza kuu la jumuiya na taasisi za kiislamu kwa pamoja wameamua kuanzisha vyama vya akiba na mikopo ambavyo vinatoa mikopo isiyo na riba.

Aidha aliwataka waumini wa dini ya kiislamu kutoutumia uislamu kuleta uhasama katika jamii bali wanapaswa kujenga na kuimarisha ustawi wa jamii kwa mustakabali wa taifa na hakuna sababu ya kuanzisha malumbano na migogoro kwa sababu ya vitu vinavyoweza kuzungumzika kwa amani na utulivu likiwemo suala la kuchinja ambalo hivi karibuni lilizua mjadala na malumbano na hata kusababisha vifo katika baadhi ya maeneo nchini.

 Akizungumzia umuhimu wa kufuata nidhamu bora za matumizi ya fedha watakazokopa kutoka kwenye chama hicho cha akiba na mikopo kilichofunguliwa mjini Songea Shekh Sanze amewataka waislamu watakaopewa mikopo kuitumia kwa nidhamu na kwa malengo yaliyokusudiwa badala ya kuitumia kwa mambo ya anasa ikiwemo kuoa bali wanapaswa kuitumia mikopo hiyo kwa shughuli za kiuchumi,ujasiriamali na elimu zaidi.
Naye mmoja wa waasisi wa baraza la wislamu(BAKWATA) Mustapha Songambele akizungumza kwenye hafla hiyo ya uzinduzi wa chama hicho cha akiba na mikopo aliwataka waislamu na wananchi kwa ujumla mkoani Ruvuma kujenga na kudumisha utamaduni wakushirikiana bila kujali imani za kidini kwa sababu suala la maendeleo halipaswi kuwa na ubaguzi wa aina yoyote.




No comments:

Post a Comment