Mwenyewe anasema mwanzoni alikuwa anajisikia aibu sana kwa kuwa na manywele marefu namna ile mpaka hapo baadaye jina na taswira ya mfalme wa reggae ulimwenguni,hayati Bob Marley ilipopata umaarufu nchini Zaire, ndipo alipoipenda staili ile ya nywele kwani hata watu wengine pia walianza kuikubali na kuionea ufahari. Pia inasemekana Remmy alizaliwa akiwa tayari na meno mawili ya mbele kitu ambacho kilichukuliwa kama ishara ya baadaye kuja kuwa mganga wa kienyeji pia. Ingawa utabiri huo haukutimia, inasemekana huo ndio mwanzo wa yeye kujulikana hapo baadaye kama Doctor Remmy Ongalla.
Baba yake ndiye aliyeanza kumfunza mambo ya muziki tangia akiwa mdogo kabisa jambo lililomfanya aamini kabisa kwamba kama jinsi ambavyo watu wengine wamezaliwa kuwa; kwa mfano, madaktari, wanasheria,waalimu, wakulima nk, yeye alizaliwa ili awe mwanamuziki. Kwa bahati mbaya baba yake huyo alifariki dunia na kumuacha Remmy akiwa na miaka sita tu akiwa tayari ameshaanza shule. Lakini kutokana na ukosefu wa fedha na kwa sababu mama yake hakuweza kuendelea kumlipia shule, Remmy ilibidi aache shule.
Ilipofika miaka ya 60, Remmy tayari alikuwa ameshajifunza mwenyewe kupiga gitaa. Mwaka 1964 ulikuwa sio mwaka mzuri kwa Remmy kwani mama yake mzazi alifariki dunia jambo ambalo lilimuacha Remmy na mzigo wa kuwalea wadogo zake kwani yeye sasa ndio alikuwa mkuu wa familia. Bila elimu na ujuzi mwingine wowote,alilazimika kuanza rasmi kujitafutia riziki kupitia muziki. Ujuzi wake wa kupiga gitaa uliongezeka kwa kasi ya ajabu kitu ambacho kilimwezesha kuwa akitumbuiza kwa kupiga ngoma na gitaa katika hoteli mbalimbali katika sehemu mbalimbali nchini Zaire akiwa na bendi yake na vijana wenzake iliyoitwa Bantu Success.
Kwa miongo kadhaa iliyofuatia Dr.Remmy Ongala alizunguka katika sehemu mbalimbali za Zaire akiambatana na kupiga na bendi kadhaa maarufu za wakati huo nchini Zaire zikiwemo Succ s Muachana na ile ya Grand Mickey Jazz nchini Uganda.
Ingawa kwa ujumla alijifunza mwenyewe kupiga gitaa, mwenyewe anakiri kwamba muziki wa kutoka nchini Cuba ambao wakati huo ulikuwa unaanza kujipatia umaarufu barani Afrika, ulimsaidia katika kupata staili ya pekee katika upigaji gitaa. Kwa upande wa uimbaji anasema uimbaji wa Joseph Kabasele na wa Franco ulimsaidia kupata style yake ya uimbaji kama tulivyoizoea.
Mwaka 1978 Remmy aliingia jijini Dar-es-salaam baada ya kuitwa na mjomba wake ili aje ajiunge na bendi maarufu ya wakati huo,Orchestra Makassy, iliyokuwa chini ya uongozi wa mjomba wake huyo, Mzee Makassy. Huo ndio ukawa mwanzo wa maisha ya Remmy nchini Tanzania. Akiwa na bendi ya Orchestra Makassy, aliandika wimbo wake wa kwanza uliojulikana kama “Siku ya Kufa”, wimbo ambao aliuandika kumkumbuka rafiki yake aliyefariki. Wimbo huo ulianza kumpatia umaarufu.
Dr.Remmy Ongala alivyo hivi sasa.
Alidumu
na bendi ya Ochestra Makassy kwa kama miaka mitatu hivi kabla ya mwaka
1981 kuhamia katika bendi ya Orchestre Super Matimila iliyokuwa ndio
inaanza kuchipukia miaka hiyo. Hiyo ilifuatia Mzee Makassy kuhamishia
bendi yake nchini Kenya. Jina la bendi hiyo, Matimila, lilitokana na
jina la kijiji kimoja kilichoko kusini mwa Tanzania. Baada ya
kujiunga kwa Remmy, bendi ya Matimila ilijiongezea umaarufu katika anga
za muziki nchini Tanzania wakati huo. Bendi hiyo kwa wakati mmoja
ilikuwa na wanamuziki kama 18 hivi ingawa kati yao wanamuziki 6 mpaka 8
tu ndio waliokuwa wanalikwaa jukwaa kufanya vitu vyao. Pamoja na hayo
kila mmoja alikuwa anapata japo nafasi ya kupanda jukwaani kuimba au
kupiga chombo/vyombo. Wakati huo ilikuwa imeshakuwa chini ya uongozi wa
Remmy Ongala ambapo pia baadaye aliiunda upya na kuibadilisha jina na
kuiita Super Matimila.Miaka iliyofuatia ilishuhudia umaarufu wa Remmy ukiongezeka hususani kutokana na mashairi ya nyimbo zake ambayo yaliegemea katika kuzungumzia mambo halisi ya kijamii kama vile umasikini, siasa nk. Mkusanyiko wa mashairi yake ulijulikana kama Ubongo au akili.
Mafanikio ya Remmy na kundi lake zima la Matimila hayakuishia nchini Tanzania kwani katika miaka ya mwishoni ya 80 walianza kujipatia umaarufu nje ya Tanzania na Afrika. Mwenyewe Remmy anasema zali la kuanza kupata mialiko ya nje lilikuja kama mchezo tu. Anasema alimpa rafiki yake mmoja mzungu aliyekuwa anaondoka nchini Tanzania kurejea kwao Uingereza kaseti yenye nyimbo zao. Rafiki yake naye alipofika huko aliwapatia jamaa wa WOMAD (World of Music,Arts and Dance) shirika linalopandisha chati wanamuziki na wasanii mbalimbali kutoka katika nchi za dunia ya tatu. Jamaa walivutiwa na nyimbo zao na hivyo kuwapa mwaliko kushiriki katika maonyesho yao barani Ulaya ya mwaka 1988.
Baada ya kurudi kutoka Ulaya bendi ya Matimila ilitoa mkusanyiko wa nyimbo zao waliouita Nalilia Mwana ambamo zilikuwemo nyimbo zilizopendwa sana kama vile Ndumila Kuwili na Mnyonge Hana Haki. Mwaka 1989 Remmy na Matimila walirudi tena Ulaya kufuatia mwaliko mwingine wa WOMAD. Ni wakati huo huo ambapo walipata nafasi ya kurekodi kwenye studio ya kisasa zaidi ambayo ilikuwa inamilikiwa na mwanamuziki maarufu aitwaye Peter Gabriel. Studio hiyo ilikuwa inaitwa Real World Studios. Matokeo yake ni nyimbo maarufu kama Kipenda Roho nyimbo ambayo inasemekana aliuimba mahsusi kwa ajili ya mkewe mzungu muingereza ambaye wakati huo tayari walikuwa wameshazaa naye watoto watatu.
Mwaka 1990, Remmy na bendi yake ya Super Matimila walirejea tena katika studio za Real World ambapo walirekodi mkusanyiko wa nyimbo ulioitwa Mambo ambao ulikuwa na nyimbo kama hiyo ya Mambo (aliimba nyimbo hii kwa kiingereza pia ili kukidhi kiu ya wapenzi wake wasiojua Kiswahili) na nyinginezo kama ule wa “No Money, No Life” na “One World”.
Umaarufu wake ulizidi mwaka 1990 alipotoa wimbo wa Mambo Kwa Socks ingawa baadhi ya watu waliupinga kwa kusema kwamba “hauna maadili” ingawa kimsingi alikuwa anawaasa watu hususani vijana kutumia kondomu ili kuepukana na maambukizi ya ugonjwa wa ukimwi.
Pamoja na yote hayo, miaka michache iliyopita Dr.Remmy Ongala aliamua kuachana na muziki wa dansi kwa madai ya kwamba umejaa mambo mengi ya kishetani. Remmy akaokoka, akatubudu dhambi zake na hivi sasa anamuimbia bwana. Mpaka hivi sasa ameshatoa albamu yake ya injili aliyooiita Kwa Yesu Kuna Furaha. Mapema mwaka huu alikuwa mbioni kukamilisha albamu yake ya pili. Bado anaishi Sinza (Kwa Remmy) mahali ambapo panaitwa hivyo kwa heshima yake.
Dr.Remmy Ongala(mwenye rasta) siku alipobatizwa.Pichani yuko na waumini wenzake.
Imeandikwa kwa msaada wa vyombo mbalimbali vya habari mtandaoni.CHANZO BongoCEBRITY
No comments:
Post a Comment